Mshambuliaji wa Man City, Raheem Sterling huenda akakaa nje ya uwanja kwa muda wa majuma manane na zaidi, kufuatia majeraha ya nyonga aliyoyapata wakati wa mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England, uliocheza mwishoni mwa juma hili dhidi ya Man Utd.

Taarifa zilizotangazwa na kituo cha televisheni cha Sky Sports, zimeeleza kwamba mshambuliaji huyo, amepata majeraha makubwa ambayo yamewalazimu wakuu wa kitengo cha utabibu cha Man City, kushauri akae nje ya uwanja kwa kipindi hicho ambacho ni sawa na kukosa sehemu ya mwisho ya msimu huu.

Tayari Sterling, ameshaondolewa katika kikosi cha timu ya taifa ya England, ambacho mwishoni mwa juma hili kitapambana na mabingwa wa soka duniani, timu ya taifa ya Ujerumani katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki na kisha Uholanzi kati kati ya juma lijalo.

Wakati taarifa hizo zikitoka, mlinda mlango wa Man City, Joe Hart ambaye pia alipata maumivu ya kiazi cha mguu wakati wa mchezo dhidi ya Man Utd, huenda akarejea uwanjani kabla ya mwishoni mwa msimu huu.

Hart amebainika hakuumia kwa kiasi kikubwa, lakini ameshauriwa kupumzika kwa majuma kadhaa, ambapo inaamiwa atakua tayari kurejea uwanjani baadae kuisaidia timu yake ambayo ipo katika wakati mgumu wa kujihakikishia nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa barani Ulaya, kwa msimu ujao wa 2016-17.

Man City Bado Wana Ndoto Za Kumnasa Lionel Messi
Licha Ya Marekebisho Ya Ratiba Ya VPL Manara Aikumbusha Tena TFF