Idara ya Uhamiaji nchini imeweka utaratibu wa kutoa kibali maalum kwa raia wa Burundi ambao wanataka kuja Tanzania kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo ikiwa ni moja ya njia za kupunguza raia wa nchi hiyo ambao huingia kinyemela hususani katika mikoa ya Kigoma na Tabora kwa ajili ya kufanya kazi za kilimo kama vibarua.
Mpango huo umetangazwa na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, Anna Makakala mwishoni mwa ziara yake iliyomfikisha katika wilaya zote na katika maeneo ya mpaka na nchi jirani ambapo amesema kuwa vibali hivyo vya miezi mitatu vitawezesha raia hao kutambuliwa na serikali kupata fedha na kutambua wako wapi na idadi yao.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamesema uamuzi huo wa idara ya uhamiaji utasadia kupunguza uhalifu na kuongeza tija katika kilimo pamoja na kujenga mahusiano mazuri na nchi jirani ya Burundi ambayo raia wake wanaongoza kwa kuja nchini kufanya vibarua bila ya kibali na hivyo kuongeza idadi ya wahamiaji haramu.