Raia wa Morocco ameondolewa nchini Urusi baada ya kuvaa fulana yenye maandishi yanayolikosoa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) na kutaka kuingia nayo uwanjani.

Kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Yassine Omairy, ambaye ni raia wa Morocco huku mmoja kati ya wazazi wake akiwa ni Mmarekani, alizuiwa kuingia uwanjani akiwa na fulana iliyosomeka ‘Shame on You Fifa (Aibu yenu Fifa).

Maandishi hayo yalitokana na hasira za mashabiki wa Morocco kufuatia maamuzi tata ya muamuzi yaliyofanywa kwenye mchezo kati ya nchi hiyo dhidi ya Ureno, wiki iliyopita.

Baada ya kushindwa kuwashawishi maafisa wa Urusi kwenye mlango wa kuingia uwanjani, alishikiliwa kwa muda na pasi yake ya kusafiria ilichukuliwa. Lakini ameiambia BBC kuwa alirejeshewa pasi yake baadaye na kuruhusiwa kuangalia kipindi cha pili dhidi ya Uhispania.

Omairy aliweka kwenye mtandao wa Facebook video inayoonesha tukio hilo, akisikika akimwambia afisa aliyemzuia kuwa, “hakuna kosa kwa maandishi haya, timu yetu ilionewa kwenye mchezo uliopita, tunaiunga mkono nchi yetu kwa kuwaambia Fifa ‘aibu yenu’… hakuna tusi hapa.”

Hii ni kwa tafsiri isiyo rasmi ya mazungumzo kwa lugha ya kiingereza kati ya afisa huyo na Omairy.

“Sasa naweza kusema sauti yetu imesikika kwa watu wengi na ujumbe wetu umefika duniani kote. Hii video sio sauti yangu pekee… hii video inawakilisha raia wa Morocco duniani kote. Mungu ibariki Morocco na aibu yenu Fifa,” aliandika kwenye video hiyo aliyoweka Facebook.

Omairy ameeleza kuwa mara tu baada ya mchezo huo alilazimishwa kuondoka nchini Urusi kurejea kwao.

Video: Hamisa afuata nyayo za Diamond, aachia ngoma yake ya kwanza 'Madam Hero'
Lennox Lewis awatolea uvivu A. Joshua, Deontay Wilder