Raia 13 wa Urusi wameshitakiwa kwa kuingilia uchaguzi mkuu wa Marekani wa mwaka 2016, kwa mujibu wa uchunguzi wa FBI.
Imeelezwa kuwa kati ya hao, watatu wanashtakiwa kwa kushirikiana kufanya makosa hayo kupitia mtandao na wengine wakiwa wamedanganya utambulisho wao na kufanya uhalifu kwa lengo la kuchakachua matokeo halisi ya uchaguzi.
Taarifa za kukamatwa kwa watu hao zilitolewa na Mkuu wa kitengo maalum cha uchunguzi nchini Marekani, Robert Mueller ambaye anasimamia uchunguzi wa madai ya Urusi kuingilia uchaguzi huo.
Katika sakata hilo, baadhi ya mashirika ya Urusi pia yametajwa kuwa miongoni mwa watuhumiwa wa kuingilia uchaguzi.
“Washtakiwa walijifanya maafisa au raia wa Marekani na kuendesha kampeni zao kwenye mitandao, wakikusanya makundi ya watu na kuwarubuni,” imeeleza taarifa hiyo.
Alisema kuwa watu hao walianza kujadili mpango wa kuchakachua matokeo ya uchaguzi huo tangu mwaka 2014.
Rais Donald Trump alishinda uchaguzi huo akimuacha kwa kura za majimbo mpinzani wake, Hillary Clinton.
Marekani imekuwa ikiituhumu Urusi kwa kuingilia uchaguzi huo, madai ambayo Urusi imeyapinga vikali.