Maandamano makubwa yamefanyika jijini Kinshasa mbele ya Ofisi ya rais wa nchi hiyo, Felix Etienne Tshisekedi kumshinikiza atimize ahadi yake ya kampeni ya kuimairisha usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Maandamano hayo yanakuja kufuatia kuuawa kwa watu saba siku ya Jumatatu katika eneo la Beni lililopo mashariki linalotazamwa kama ngome ya uasi.

Zaidi ya raia mia moja kutoka eneo hilo la mashariki ya Congo waliandamana mbele ya Ofisi ya rais, Felix Tshisekedi jijini Kinshasa, wakilalamika kuwa kiongozi huyo anashindwa kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu.

Changamoto kubwa inayomkabili rais Tshisekedi tangu alipoingia madarakani ni kutathmini jinsi gani ataweza kuleta amani katika eneo hilo la mashariki ya nchi hiyo ambako kumeshuhudiwa ghasia na umwagikaji damu mkubwa wa raia, na uwepo wa Wanamgambo waliojihami wanaotekeleza mashambulio.

”Tumemuomba Rais wa Congo, Felix Tshisekedi atusaidie, tumeteseka sana huko Beni, kila siku watu wanauawa, tunaandamana kwa sababu ndugu zetu wamekufa, watoto wamebaki yatima, rais alifika huko alisema atamaliza vita lakini hakufanya kitu, tumesema siku nyingi sana tangu aingie madarakani, lakini hajafanya chochote,”amesema raia mmoja aliyekuwa katika maandamano hayo

Aidha, raia hao walioandamana walisindikizwa na baadhi ya wabunge waliochaguliwa kutoka jimbo la Beni lililopo mashariki mwa nchi hiyo, ambapo wabunge hao wamesema kuwa kuna ripoti ambayo waliwaandikia viongozi wa nchi kuhusu hali hiyo lakini mpaka sasa ripoti hizo zinafichwa ndani ya kabati za ofisi.

Hata hivyo, ripoti iliyotolewa Jumatano Agosti 14 na Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch inaeleza kuwa watu 1900 waliuawa na wengine 3300 walitekwa nyara na vikundi vya watu walio na silaha katikati ya Juni 2017 na Juni 2019.

 

 

Mke na Mume wahukumiwa kwenda jela miaka mitano
Dkt. Slaa alalamikia wapinzani kuichafua nchi, Lissu amjibu