Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), waandamanaji wamevamia vituo vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo (MONUSCO), kilichopo mji wa Goma jimbo la Kivu Kaskazini na kupora mali, kurusha mawe na kuchoma moto matairi ya magari.
Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq akizungumza na waandishi wa habari jijini New York nchini Marekani Julai 25, 2022, amesema waandamanaji hao walilenga vituo vya MONUSCO vilivyopo Goma na kuweka vizuizi barabarani na Wanajeshi kadhaa walijeruhiwa.
Licha ya Walinda amani kulazimika kufyatua mabomu ya kutoa machozi na risasi za maonyo kwa ajili ya kulinda wafanyakazi na hospitali ya Umoja wa Mataifa na miundombinu mingine muhimu, bado hali haikuwa shwari kutokana na wengi wao kuwa na hasira.
Haq amesema, tukio kama hilo pia limetokea katika kituo cha MONUSCO kilichopo Nyamilima umbali wa kilometa 38 kaskazini-mashariki mwa mji wa Rutshuru ambapo eneo la Kitchanga, kilometa 28 kaskazini-mashariki mwa mji wa Masisi maandamano yakifanyika kwa amani.
Taarifa ya MONUSCO iliyotolewa leo kwenye mji mkuu wa DRC Kinshasa, imelaani matukio hayo ikisema, “maeneo ya Umoja wa Mataifa hayapaswi kuvamiwa kwa mujibu wa makubaliano kati ya Umoja wa Mataifa na serikali ya DRC kuhusu hadhi ya majeshi.”
Wakati huo huo, MONUSCO imeanza kutumia itifaki za nyongeza za usalama ikiwemo kuweka mikakati ya kuendana na mazingira, itahahakikisha utekelezaji wa mamlaka yake ya usalama na ulinzi wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa unakuwa shwari.