Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limesema kuwa raia mmoja kati ya watatu nchini Burundi anahitaji msaada wa kiutu.
Muwakilishi wa shirika hilo nchini Burundi, Garry Conille amesema kuwa mahitajhi ya watu wa Burundi yamesababishwa na hali mbaya ya kisiasa ambayo imepelekea kushuka kwa kiuchumi na kuongezeka kwa majanga asilia.
Ameongeza kuwa matatizo kama hayo yamesababisha hali ya maisha kuwa mbaya zaidi, kufikia huduma za msingi kuwa tatizo na pia kusababisha idadi kubwa ya watu kukosa makazi yao.
“Tathmini ya mahitaji ya misaada ya kiutu ya taifa la Burundi inaonyesha kuwa watu milioni 3.6 ambao ni theluthi moja ya idadi ya jumla ya watu nchini humo watahitaji msaada huo mwaka huu, hali inayoashiria ongezeko la asilimia 20 ikilinganishwa na mwaka jana,”amesema Conille
Kwa mujibu wa makadirio ya UNDP serikali hiyo itapokea dola milioni 141 sawa na Yuro milioni 115 kushughulikia mahitaji hayo mwaka huu.