Wakati mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu nchini Kenya ukiendelea, mgombea urais anaeungwa mkono na muungano wa vyama vya upinzani wa National Super Alliance (NASA), Raila Odinga ameweka wazi kama atakubaliana na matokeo yatakayotangazwa na Tume ya uchaguzi ya IEBC.
Mwanasiasa huyo ambaye aliyakataa matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2007 alipochuana na rais mstaafu wa Kenya, Mwai Kibaki hali iliyopelekea nchi hiyo kuingia kwenye vurugu kubwa, alisema kuwa mwaka huu yuko tayari kuyakubali matokeo ya uchaguzi huo endapo atatangazwa kushindwa.
Raila aliyasema hayo hivi karibuni alipofanya mahojiano na kipindi cha Jambo Kenya cha Redio Citizen lakini aliweka masharti na vigezo vya kuyakubali matokeo hayo kuwa ni lazima IEBC ihakikishe uchaguzi umekuwa huru na wa haki.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa muungano wa NASA alikosoa Serikali akidai kuwa inatumia vikosi vya jeshi la ulinzi la nchi hiyo (Kenya Defense Force) katika mchakato wa uchaguzi kinyume cha katiba kwani kazi hiyo inapaswa kufanywa na jeshi la polisi.
Mwanasiasa huyo nguli alidai kuwa serikali imekuwa ikitumia vibaya rasilimali za nchi hiyo kwani jeshi la ulinzi linapaswa kufanya kazi ya kulinda mipaka ya nchi na sio kupambana na wananchi. Aliongeza kuwa Rais Uhuru Kenyatta kama Amiri Jeshi Mkuu amekuwa akivuka ukomo wa madaraka yake.
“Nimesikia hivi karibuni kuwa kuna kikao kinaendelea katika makazi ya jeshi ya Embakasi, ambacho kinahusisha wafanyakazi wa serikali kama waratibu wa mikoa na wilaya, viongozi wa ngazi za juu wa polisi na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la ulinzi, walikuwa wakijadili namna ya kuweka ulinzi wakati wa uchaguzi,” Raila anakaririwa na Citizen.
“Lakini nikasema hili ni kinyume cha katiba, kulihusisha jeshi la ulinzi kwenye masuala ya ndani ya nchi,” aliongeza.
Aidha, mgombea huyo wa urais alimtaka mpinzani wake, Rais Kenyatta pia kuweka wazi kuwa atakubali matokeo ya uchaguzi endapo atashindwa na kwamba asiingilie mchakato wa uchaguzi.
Kenya inatarajia kufanya uchaguzi mkuu Agosti 8 mwaka huu, katika uchaguzi ambao unatajwa kuwa wa mchuano mkali katika historia ya chaguzi za nchi hiyo huku muungano wa upinzani wa NASA ukichuana vikali na muungano wa chama tawala wa JUBILEE.