Mgomnbea urais wa Kenya, Raila Odinga ametoa ufafanuzi wake kuhusu uamuzi wa kuyakataa matokeo ya uchaguzi yanayoendelea kutangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo (IEBC).
Akizungumza hivi punde na waandishi wa habari, Odinga aliyeongozana na wataalam wa mifumo ya TEHAMA na viongozi wengine waandamizi wa NASA, alisema kuwa mfumo wa kuhifadhi kumbukumbu (data base) ya IEBC ulidukuliwa mara kadhaa na watu ambao walikuwa wanabadili matokeo ya kura kadiri wawezavyo.
Odinga amesema kuwa timu yake ya wataalam imeweza kubaini na kwamba inavyo vielelezo vinavyoonesha ni nani ambaye aliingia kwenye mfumo huo na muda alioingia na alichokifanya kwa wakati huo.
Ngome hiyo ya NASA imeeleza kuwa itasambaza vielelezo vyote kwa waandishi wa habari ili Wakenya waweze kuona nini kilichofanyika kwenye udukuzi huo.
Mwanasiasa huyo mkongwe amedai kuwa udukuzi huo ulifanyika kuanzia majira ya saa sita usiku hadi majira ya saa kumi alfajiri.
“Naomba kuwaeleza Wakenya kwamba tumeweza kubaini uchakachuaji wa kura uliofanywa na upande wa Jubilee, waliingia kwenye mfumo na kubadili matokeo wakimuongezea mpinzani wetu. Hii imefanyika kwa kaunti zote 47,” alisema Odinga.
“Vilevile imebadili matokeo sio ya uraisi peke yake, bali pia ni ya Wabunge, Maseneta na Magavana. Wizi huu haujawahi kufanyika tangu tuanze mfumo wa siasa za vyama vingi. Na waliofanya haya mambo wanajulikana,” aliongeza.
- Wizara ya Ardhi yabuni mbinu mpya za ulipaji kodi pango la ardhi
- Odinga apinga matokeo yanayoendelea kutangazwa
Aliwataka Wakenya wawe watulivu wakati NASA inafikiria hatua za kuchukua dhidi ya kile anachodai ni wizi wa aina yake.
Alisema kuwa leo watakutana na waangalizi wa uchaguzi huo kutoka mataifa mbalimbali ili waweze kuwapa vielelezo vyao na kuwaeleza madai yao.
Kwa upande wa Jubilee, mapema leo wamemshukia Odinga wakidai kuwa anataka kuwachanganya Wakenya na malalamiko yasiyo na msingi kwani fomu namba 34A ni ya kidijitali.
Kwa mujibu wa matokeo yanayosambazwa na IEBC, Kenyatta anaongoza akiwa na asilimia 54.44 dhidi ya Odinga ambaye ana asilimia 44.71, kukiwa na tofauti ya kura zaidi ya milioni moja.