Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga ameeleza sehemu ya mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni rafki yake wa siku nyingi, Dkt John Magufuli.

Akizungumza hivi karibu ni jijini Dar es Salaam, Odinga amesema kuwa alikutana na Rais Magufuli Agosti 14 mwaka huu Ikulu jijini Dar es Salaam na kupata chakula cha jioni pamoja.

Alisema kuwa alimuuliza Rais Magufuli kuhusu kile alichosikia kuwa amezuia viongozi wa ngazi za juu wa kitaifa vya upinzani, walioshindwa kufanya mikutano ya hadhara au kuvuka jimbo waliloshinda kwenda lingine na majibu aliyopewa ni tofauti na kile alichokuwa akisia kikisemwa nje.

“Anasema hajakataza, kama wakifanya eneo lao wanaweza kufanya, lakini kubeba watu kutoka jimbo hili kwenda jimbo lile kwa mabasi kwenda kufanya vurugu ndio amesema amekataa,” Odinga ameliambia gazeti la Mtanzania.

Wahariri wa gazeti hilo walimdadisi zaidi Odinga wakitaka kujua kama Rais Magufuli alimueleza kuhusu msimamo wake wa kupiga marufuku siasa za ushindani hadi 2020.

“Anasema hajakataza,” alijibu huku akimalizia kwa kicheko.

Alisema kuwa kazi ya upinzani ni kupinga na sio kushangilia na kwamba hiyo ndio demokrasia.

Katika hatua nyingine, Raila Odinga alithibitisha kuwa atajitosa kuwania urais nchini Kenya na kwamba anaamini watashinda.

Alisema kuwa wanazo rekodi zinazoonesha kuwa katika uchaguzi Mkuu uliopita nchini Kenya, Serikali iliyoko madarakani haikushinda nafasi ya Urais.

Anasema kuwa hilo lilithibitishwa na idadi iliyotajwa ya watu milioni 10 waliotajwa kupiga kura ya kuwachagua Maseneta, Magavana, Wawakilishi, Madiwani n.k, huku tume ikitaja idadi ya waliomchagua rais kuwa ni milioni 12.

Mwanasiasa huyo alihoji ilipotolewa idadi ya watu milioni 2 waliopiga kura ya kumchagua rais tu.

Alisema kuwa tayari wamefanikiwa kushawishi kwa kukusanya saini, kufanya maandamo na hatimaye mazungumzo na Serikali yaliyopelekea kukubaliana kuvunja Tume ya Uchaguzi na kuunda Tume mpya itakayosimamia uchaguzi wa mwakani.

Chadema Watangaza Safu ya Maandamano ya UKUTA.......Lowassa Amepangiwa Mbeya, Katibu Mkuu Kapangiwa Mwanza
Ndege Ndefu Kuliko Zote Duniani Yapaa Uingereza