Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC, Felix Thisekedi amehusisha athari za mabadiliko ya tabinachi na mafuriko makubwa yaliyolikumba taifa lake na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 100 katika mji mkuu wa Kishansa.
Mafuriko hayo, pia yalisababisha Barabara kuu kufungwa katika jiji hilo lenye wakazi milioni 15 ambapo kufuatia msiba huo Ofisi ya Waziri Mkuu, Jean-Michel Sama Lukonde kutangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa.
Mkuu wa jeshi la Polisi wa DRC, Sylvano Kasongo amesema wengi wa waliofariki walikuwa wakiishi katika maeneo ya milimani ambako kulikumbwa na maporomoko ya udongo.
Aidha, Tshisekedi ambaye yupo jijini Washington amemwambia waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Anthony Blinken wakati wa mkutano kati ya Marekani na viongozi wa Afrika, kwamba DRC inakabiliwa na shinikizo kubwa, lakini ni bahati mbaya hakuna anayesikia wala kuisaidia.
Hata hivyo, jiji la Kinshasa lina changamoto ya miundombinu na idadi kubwa ya watu, huku Tshisekedi akisema ni lazima mataifa yanayochafua mazingira kutoa msaada, kwa kuwa hayo ndio chanzo cha uharibifu na athari kwa mataifa masikini yanayoshindwa kujilinda dhidi ya athari za mabadiliko.