Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi amelaani jaribio la mauaji ya halaiki katika eneo la jimbo la Kaskazini kufuatia vifo vya mamia ya watu katika eneo hilo huku maelfu wakiyakimbia makazi yao.
Akizungumza jana alipolihutubia taifa hilo, Rais Tshisekedi alisema kuwa mauaji ya watu 160 yaliyofanywa na kundi la wapiganaji wenye silaha tangu Juni 10 mwaka huu katika eneo hilo yanapaswa kukomeshwa mara moja.
Aliagiza jeshi la nchi hiyo kufanya oparesheni kubwa katika maeneo hayo kwa lengo la kufuta makundi ya watu wenye silaha yanayotekeleza mauaji hayo.
“Kwa hakika, hili ni jaribio la mauaji ya halaiki, kiufanya nchi yetu iwe katika moto,” alisema na kuongeza kuwa lengo la washambuliaji hao ni kuifanya nchi hiyo kukosa amani muda wote.
Wakala wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi, alisema kuwa taharuki iliyoletwa na washambuliaji hao imesababisha zaidi ya watu 300,000 kuyahama makazi yao, wengi wakitokea eneo la Djugu.
Juni mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulitoa tamko la kulaani vitendo vinavyofanywa na washambuliaji hao na kueleza kuwa imeshuhudia mashambulizi kadhaa yakihusisha makundi ya Hema na Lendu.
Rais Tshisekedi ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu amesema kuwa oparesheni itakayofanywa na jeshi la nchi hiyo italenga katika kukomesha kabisa vitendo hivyo katika maeneo ya Djugu, Mahagi kuelekea katika jimbo la Kivu Kusini ambako makundi ya waasi yamekuwa yakinyemelea utajiri wa madini katika eneo hilo.