Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameonesha hali ya kuwashangaza wakenya pamoja na ulimwengu baada ya kumnyima kipaza sauti Naibu wake wa Urais William Ruto ili kuhutubia wakati wa sherehe za Madaraka zilizofanyika Juni Mosi bustani ya Uhuru.
Katika itifaki ya kawaida, Naibu rais William Ruto ndiye huzungumza na kisha kuwaalika Rais lakini katika sherehe hizo mambo yakawa tofauti ambapo Rais ndiye alichukua jukwaa baada ya shamrashamra za kutumbuiza wageni kukamilika na akaanza kuhutubu.
Rais Kenyatta alimpa nafasi Rais wa Sierra Leon Julius Maada na baada ya mgeni huyo kukamilisha hotuba yake Rais Uhuru akachukua nafasi tena.
Aidha wakati wote huu, DP Ruto alionekana kwenye jukwaa huku akiwa amejituliza kando ya Mama Margaret Kenyatta ambaye ni mke wa Rais Kenyatta.
Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa kisiasa walikuwa tayari wameona dalili za DP Ruto kupotezwa jukwaani kwani hata mfawidhi wa hafla hiyo hakutambua kufika kwa DP Ruto uwanjani na Rais Uhuru pia alikosa kumzungumzia naibu wake wakati wa kutambua wageni waliokuwa wamefika kwenye sherehe hizo.
Rais Kenyatta pia katika hotuba yake alimpigia debe muungano wa Raila Odinga na Martha Karua akisema wakenya sasa wana nafasi ya kumchagua mama na alikashifu wandani wa DP ambao wamekuwa wakimkosoa akisema serikali yake imefaulu kupiga hatua za miradi mikubwa kwa sasa.
Aidha wakati wa kuondoka, Rais alitembea na Mama Margaret Kenyatta na kumwacha DP Ruto bila wao hata kusemezana hali ambayo haikuwa ya kawaida.
Wafuasi wa DP Ruto wamekerwa na hatua hiyo wakisema ilikuwa ni dharau kubwa kwa naibu wake na wakenya wengi wameendelea kuhusisha tukio hilo na kudhoofika kwa uhusiano wa kisiasa kati ya viongozi hao wawili wa serikali.