Rais Daniel Ortega wa Nicaraguan amemteua mkewe, Rosario Murillo kuwa mgombea mwenza wake kwa lengo la kuwa Makamu wake wa Rais kupitia uchaguzi mkuu utakaofanyika Novemba mwaka huu.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa nchini humo wanampa nafasi kubwa Rais huyo kuwa mshindi wa uchaguzi huo utakaomfanya kuendelea kuongoza nchi hiyo kwa awamu ya tatu mfululizo.

Ortega mwenye umri wa miaka 70 ameeleza kuwa amemchagua mkewe kwa lengo la kuweka usawa wa kijinsia katika Serikali yake na kwamba ilibidi amuweke mtu anayemjua vizuri kwa utendaji wake wa kazi.

“Hatuna shaka kwamba makamu wa Rais anapaswa kuwa mwanamke, ambaye ni zaidi ya mwenza, ambaye ameshajaribiwa vya kutosha kwa kazi na akathibitika kuwa ni mfanisi na mtiifu,” alisema Rais Ortega Jumanne ya wiki hii alipokuwa akiwahutubia wafuasi wa chama chake.

Vyama vya upinzani vya nchi hiyo pia vimetangaza kusimamisha wagombea kadhaa lakini utafiti uliofanywa hivi karibuni nchini humo unampa ushindi wa asilimia 65 Rais Ortega na wabunge wake huku akiwaacha kwa mbali sana wagombea wa vyama vingine.

Mke wa Rais huyo ni mwandishi maarufu wa mashairi na mwana mapinduzi aliyesaidia katika harakati za ukombozi wa mwaka 1979 akiwa na chama cha Sandinista National Liberation Front, ambacho sasa ndicho chama tawala kilichobadili jina.

Mwanamke huyo ambaye pia ni mwanasiasa mkongwe aliyefunga ndoa na Rais Ortega mwaka 1985, amekuwa msemaji wa Serikali hiyo na kushina nafasi ya Uwaziri.

Cristiano Ronaldo Kusaini Mkataba Mpya
Video: Tamko la TECMN kuhusu taarifa ya Serikali ya kukata rufaa kesi ya kupinga ndoa za utotoni