Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi hii leo Septemba 2, 2022 amekubali barua ya kujiuzulu ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu uchumi Zanzibar (ZAECA), ACP Ahmed Khamis Makarani.
Hatua hiyo inatokana na maelekezo ambayo Rais Mwinyi aliyatoa kwa kuitaka ZAECA kujitathmini baada ya hivi karibuni kupokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG Dkt. Othman Abass Ali.
Ripoti ya hiyo ya CAG, ikianika madudu na ubadhirifu wa fedha za umma, ambapo Rais Mwinyi aliinyooshea kidole kwa kusema kuwa haina msaada kwa Serikali na kusema kama mamlaka zinazohusika zingekuwa zinafanya kazi, kungekuwa hakuna marudio ya madudu.
Dk Mwinyi alisema katika ripoti ya mwaka jana ilionesha uwepo wa wizi mkubwa na wa wazi unaotokea Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Afya na Mamlaka ya Mapato Zanzibar, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.
“Baadhi ya watu walihusishwa na kukiri kuchukua fedha, lakini hakuna hatua wala kusikia mtu hata mmoja aliyefikishwa mahakamani. “Kuna fedha zilizotolewa na Wizara ya Kilimo za ununuzi wa mbolea kinyume kabisa, lakini hakuna hatua za kisheria zilizochukuliwa,” alisema Dkt. Mwinyi.
Aidha, alifafanua kuwa, “lakini CAG endelea kusema ukweli, yapo mengine yana majibu, mengi hayana na huu ndio utakuwa utaratibu wetu wa kila mwaka, lazima tuweke ripoti hizi wazi na huo ndio utawala bora.”
Ripoti hiyo ya CAG, ya vitabu sita vyenye ripoti 182 ambazo zinajumuisha Serikali Kuu, mamlaka za Serikali za mitaa na mashirika ya umma, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Afya na Kilimo, zilipata hati chafu kutokana na uwepo wa ubadhirifu mkubwa wa fedha.
Kuhusu Wizara ya Afya, CAG alisema zipo zabuni zilizotolewa na kuonekana wanaidai wizara lakini kiuhalisia ni tofauti na madai yao na kwamba baadhi ya dawa ziliagizwa kwa gharama kubwa na baada ya muda mfupi zilikwisha muda wake.
Aidha, Dkt. Ali aliongeza kuwa, Serikali ilikadiria kupokea Sh24 bilioni ikiwa ni gawio kutoka katika mashirika yake mbalimbali, lakini hadi kufikia Juni mwaka huu gawio halisi ni Sh15.4 bilioni, sawa na asilimia 64 ya makadirio.