Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amesema kuwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utafanyika ndani ya miezi mitano ijayo.
Mnangagwa amekaririwa na shirika la habari la Reuters alipokuwa katika ziara yake nchini Msumbijji ambapo ameahidi kuwa uchaguzi huo utakuwa huru na haki na kwamba kinachoangaliwa zaidi ni amani ya nchi hiyo.
Rais huyo ambaye alichukua nafasi ya Robert Mugabe mwishoni mwa mwaka uliopita anatarajia kushiriki katika uchaguzi huo kwa tiketi ya chama tawala cha Zanu-PF.
“Tutahakiksha kuwa uchaguzi unakuwa huru, haki na wenye hadhi ya uchaguzi ili kuihakikishia dunia kuwa Zimbabwe sasa ina vigezo vya kuitwa nchi ya kidemokrasia.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zimbabwe, uchaguzi unapaswa kufanyika kati ya Julai 22 na Agosti 22 mwaka huu. Lakini Bunge linaweza kuharakisha zaidi endapo litavunjwa mapema.
Kwa mujibu wa Reuters, chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change kimedhoofika na kugawanyika kwa sababu kiongozi wake Morgan Tsvangirai aendelea kupata matibabu ya ugonjwa wa Saratani hivyo hashiriki harakati za kisiasa.