Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezitaka sekta za Serikali kushirikiana katika kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuleta mafanikio na mabadiliko kwa haraka.
Rais Samia ameyasema hayo hii leo Juni 6, 2022 mara baada ya kushuhudia utiaji saini mikataba ya miradi ya maji ya miji 28 ya Tanzania.
Aidha Rais Samia ameipongeza Wizara ya Maji kwa kushirikiana vyema na watendaji wengine kumalisha hatua hiyo muhimu.
“Nakupongeza Waziri wa Maji na timu yako kwa kufanikisha suala hili muhimu na kuwahakikishia wananchi kuwa mradi huu utainufaisha miji yote 28 na hakuna mji ambao utaachwa,” amepongeza Rais Samia.
Amesema, “Sekta za Serikali fanyeni kazi kwa kushirikiana kama walivyofanya Wizara ya Maji na Fedha, ushirikiano ukiwepo kazi zitaenda kwa haraka na wananchi watanufaika na kazi tunazozifanya”.
Hata hivyo, ameiasa Wizara hiyo kuendelea kutekeleza vipaumbele vilivyopo na kwamba wanatakiwa kujipanga vyema ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Hongereni kwa sababu Wizara hii mmebadilika sana, mwanzoni hali ilikuwa mbaya lakini kwa sasa mambo yanakwenda vizuri, Mradi huu ilikuwa utekelezwe kwenye miji 16 lakini umekwenda hadi miji 28, pia niwapongeze kwa kubana matumizi hata kwa miradi mingine inayotekelezwa tofauti na huu,”
Aidha amewataka Wahandisi wa Wizara kusimamia hatua zote za maradi huo kwani fedha za ujezi wake zimetokana na mkopo, hivyo zikamilishe ujenzi na maji yapatikane kama inavyotarajiwa.
Awali akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Maji Jumaa Aweso, amemuhakikishia Rais Samia kuwa watendaji wote wa Wizara wana ari ya kazi na usimamizi utakua wa uhakika ili kutekeleza azma ya kumtua mama ndoo kichwani.
“Mradi huu tutausimamia na kuufuatilia usiku na mchana ili kuhakikisha yale maelekezo na matumaini ya kumtua mama ndoo kichwani yanatimia,” amesema Aweso.
Ameongeza kuwa, “Kwa miaka yote, Bajeti ya Wizara ya Maji huwa inatekelezwa kwa asilimia 50 mpaka 60, lakini ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wako, Bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka 2021/22 tumetekeleza kwa asilimia 95.”
Maji si sehemu ya kundi la chakula yakiwa na umuhimu kiafya katika kufanikisha kazi mbalimbali mwilini ikiwemo kusaidia viungo vya mwili viweze kufanya kazi vizuri, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya uzito wa mwili wa binadamu ni maji.