Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema serikali yake haitaingilia kati hali ya sasa ya uchumi
wa nchi hiyo wala suala la kupanda kwa gharama ya maisha.
Museveni ameyasema hayo kupitia hotuba yake ya kitaifa aliyoitoa kupitia Luninga Mei 22, 2022
na kusema ruzuku ya serikali au kuondolewa kwa ushuru wa uagizaji bidhaa kutaporomosha
uchumi wa Uganda.
Bei za bidhaa za petroli, malighafi na vyakula vinavyoagizwa kutoka nje nchini humo zimekuwa
zikipanda katika miezi ya hivi karibuni hali ambayo imeyakumba mataifa mengi Ulimwenguni.
“Uganda itahitaji kutotumia pesa vibaya kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na itafanya mambo
inayoweza kuyamudu na ununuzi wa bidhaa ghali ni matumizi mabaya ya pesa,” amesema
Museveni.
Aidha kupitia hotuba hiyo amewashauri wananchi wake kubadilisha ngano kutoka nje na vyakula
vinavyopatikana Uganda kama vile mtama, mahindi, ndizi mbichi na mihogo.
“Nadhani mnaelewa sehemu kubwa ya hii nchi ina mahitaji makubwa na familia nyingi
zinategemea kilimo cha kujikimu sasa tutumie mazao yetu kutunufaisha,” ameongeza Rais
Museveni.
Bei za vyakula vinavyozalishwa nchini Uganda zimekuwa zikipanda hasa maeneo ya mijini
kutokana na gharama za usafirishaji na baadhi ya raia hulazimika kununua kiasi kidogo cha vitu
vya msingi au kuegesha magari yao ili kukabiliana na hali hiyo.
Nchi hiyo inakabiliwa na mfumuko wa bei wa asilimia 4.9, ambao ni wa juu zaidi kuwahi kutokea
tangu mwaka 2017.