Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Dkt. Walid Amani Kaburu na kusisitiza kuwa amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa.
Rais Dkt. Magufuli ametoa salamu hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga baada ya kupokea taarifa za kifo cha Dkt. Kabourou aliyekuwa anatibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbuili Jijini Dar es Salaam kilichotokea usiku wa kuamkia leo Machi 07, 2018.
“Kwa masikitiko nimepokea taarifa ya kifo cha Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma Dkt. Walid Amani Kabourou kilichotokea usiku wa kuamkia leo. Dkt. Walid Amani Kaburu atakumbukwa kwa mchango wake alipokuwa kiongozi katika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM, na alipokuwa Mbunge wa Kigoma Mjini na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki,”amesema Rais Magufuli.
Hata hivyo, pamoja na salamu hizo Rais Dkt. Magufuli ameiomba familia ya marehemu na wote walioguswa na msiba huo kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi.