Katika kuhakikisha tatizo la migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima ianpatiwa ufumbuzi nchini na kuondokana na tatizo hilo, Rais Dkt. John Magufuli amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wafugaji wote wanaodaiwa kuhusika katika matukio ya kuwashambulia kwa viboko wananchi wa Kijiji cha Fukayosi kilichopo Wilayani humo.
Dkt. Magufuli ametoa agizo hilo alipokuwa safarini kutoka Dodoma kuelekea Dar es salaam mara baada ya kusimama kuwasalimia wananchi wa kijiji hicho, ambao walikuwa wamekusanyika katika kando ya Ofisi ya Kata hiyo.
Aidha, Wananchi hao walikuwa wamekusanyika huku wakiwa wameshika mabango yaliyoandikwa ujumbe wa kutaka wafugaji wa jamii ya Wamang’ati waondolewe na kisha akatoa nafasi kwa baadhi yao kueleza dukuduku lao.
Katika malalamiko ya Wananchi hao ambao ni wakulima na mfugaji mmoja aliyejitokeza kueleza kuwa Wamang’ati wamekuwa wakiwanyanyasa kwa kuingiza mifugo katika mashamba yao ya mazao na wakithubutu kuwakataza wamekuwa wakichapwa viboko na baadhi yao kuuawa.
Kufuatia malalamiko hayo, Rais Dkt. Magufuli amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaji Majid Mwanga kukomesha mara moja vitendo vya wafugaji kuwapiga wakulima na wakulima kuwapiga wafugaji, na pia kukomesha vitendo vya wafugaji kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima.
“Kuanzia leo isitokee mfugaji kumpiga mkulima, mkulima kumpiga mfugaji wala mfugaji kulisha mifugo yake kwenye mashamba ya wakulima, na suala hili nitalifuatilia mimi mwenyewe.
Hata hivyo, Rais Dkt. Magufuli amemwagiza Mkuu wa Wilaya na Viongozi kulishughulikia suala hilo kabla ya yeye hajaanza kulishughulikia.