Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi anatarajia kufanya ziara jijini Washington DC nchini Marekani mwezi Aprili mwaka huu kwaajili ya kujadili jinsi ya kuimarisha uchumi na usalama.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Robert Palladino amesema kuwa, Tshisekedi atatembelea Washington DC tarehe 3 hadi 5 mwezi Aprili na kufanya mikutano na waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo pamoja na maafisa wengine wa juu wa utawala wa Trump.
Aidha, katika taarifa hiyo iliyotolewa na msemaji huyo, haijabainisha mara moja kama rais wa DRC, Felix Tshisekedi atakutana na Rais wa nchi hiyo Donald Trump kwaajili ya mazungumzo.
“Tunaungana na matakwa ya rais Tshisekedi ya kutaka kujenga uhusiano thabiti kati ya Marekani na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, tunamkaribisha sana ili tuweze kuimarisha na kudumisha uhusiano wetu,”amesema Palladino
Hata hivyo, amesema kuwa suala la kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kulikogubikwa na vita litakuwa ni moja ya mambo yatakayojadiliwa.