Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka la Hispania, Luis Rubiales, amefungiwa kutojihusisha na soka kwa muda wa miaka mitatu kwa sababu ya kumpiga busu la mdomoni mchezaji wa kike baada ya fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake 2023, FIFA imetangaza.
Kamati ya Nidhamu ya FIFA hapo awali ilikuwa imemsimamisha Rubiales kwa siku 90 baada ya kitendo chake kumbusu Mshambuliaji Jenni Hermoso kwenye midomo, wakati Hispania ilipotwaa Kombe la Dunia kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya England mjini Sydney Agosti 20, mwaka huu.
Rubiales awali alikataa kuitikia wito wa kujiuzulu, lakini baada ya FIFA kumsimamisha kazi, Serikali ya Hispania ilijaribu kumtaka aondolewe kwenye wadhifa wake na Hermoso akawasilisha malalamiko yake na alijiuzulu Septemba 10, mwaka huu.
“Kamati ya Nidhamu ya FIFA imemfungia aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF), Luis Rubiales, kwa miaka mitatu kujihusisha na masuala ya soka katika ngazi ya kitaifa na kimataifa baada ya kubaini kuwa alikiuka kifungu cha 13 cha FIFA. Kanuni za Nidhamu,” FlFA ilisema katika taarifa yake.
“Kesi hii inahusiana na matukio yaliyotokea wakati wa fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake la FIFA mnamo Agosti 20, 2023, ambapo Rubiales alikuwa amesimamishwa kwa muda wa siku 90 awali.
“Rubiales amejulishwa kuhusu masharti ya uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya FIFA. Kwa mujibu wa vifungu husika vya Kanuni ya Nidhamu ya FIFA, ana siku kumi za kukata rufaa. FIFA inasisitiza dhamira yake kamili ya kuheshimu na kulinda uadilifu wa watu wote na kuhakikisha kuwa kanuni za msingi za maadill mema zinafuatwa.
Rublales alisema atatumia haki yake ya kukata rufaa, akiituhumu FIFA kwa kutompa nafasi ya kujitetea.