Rais na Mmiliki wa Klabu Bingwa nchini Guinea Horoya AC Mamadou Antonio Souaré, ametangaza dau Shilingi Milioni 100 na zaidi kwa wachezaji wa Klabu hiyo, endapo wataifunga Raja Casablanca ya Morocco.
Miamba hiyo ya Afrika itakutana Jumanne (Machi 07) mjini Conakry katika Uwanja wa Generali Lansana Conte kwenye mchezo wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Souaré ametoa ahadi hiyo kwa wachezaji, kwa kutambua kikosi cha Horoya AC kinahitaji ushindi kwenye mchezo huo, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutinga Robo Fainali.
Ahadi iliyotangazwa na kiongozi huyo ni kulipia Shilingi Milioni 100 kwa kila bao litakalofungwa katika mchezo dhidi ya Raja Casablanca, ambao utaanza kuchezwa saa moja jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Souaré ametamka wazi kuwa Jumanne ya juma lijayo wana kazi moja tu ya kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Raja Casablanca, ambayo ilishinda katika mchezo uliopita mabao 2-0.
Hata hivyo Horoya AC imewahi kuifunga Raja Casablanca kwenye michuano hiyo msimu uliopita Hatua ya Makundi, ikishinda 2-1 nyumbani, Uwanja wa Generali Lansana Conte.
Mchezo wa kwanza uliopigwa Morocco, Raja Casablanca ilifunga Horoya AC 0-1.