Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Joseph Magufuli amekubali ombi la kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa mzunguuko wa 29 wa ligi kuu ya soka Tanzania bara, utakaochezwa mwishoni mwa juma hili Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, kati ya mabingwa wa Tanzania bara Wekundu Wa Msimbazi Simba dhidi ya Kagera Sugar, kutoka mkoani Kagera.
Shirikisho la soka nchini TFF kupitia wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo inayoongozwa na Harrison Mwakyembe, walimuandikia barua Rais Magufuli ya kumuomba kuwa mgeni rasmi katika mchezo huo, ili akabidhi kombe la ubingwa kwa Simba.
Katibu mkuu wa shirikisho hilo, Wilfred Kidau amezungumza na waandishi wa habari, na kuthibitisha kupata jibu kutoka kwa Rais Magufuli la kukubali kuwa mgeni rasmi katika mchezo huo.
Kidau amesema Rais Magufuli kabla ya kuwakabidhi Simba kombe la ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2017/18, ataanza kukabidhiwa Kombe la ubingwa wa michuano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (CECAFA U17), ambalo Tanzania ilitwaa mwishoni mwa mwezi uliopita nchini Burundi.
Wakati huo huo Kidau amefikisha salamu za Rais Magufuli za kuitakia kila la heri Young Africans ambayo leo jioni itakua na kibarua cha kucheza mchezo wa mzunguuko wa pili hatua ya makundi, kombe la shirikisho la soka barani Afrika CAF dhidi ya mabingwa wa soka kutoka nchini Rwanda Rayon Sport ya Rwanda.