Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Paul Kagame amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku 2 hapa nchini Tanzania na kurejea nchini kwake, baada ya hapo jana kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Rais Kagame ameagwa na mwenyeji wake Rais Magufuli.
Aidha, mara baada ya kuagana na mgeni wake, Rais Magufuli amesalimiana na wananchi wa Dar es Salaam waliokuwa wamejitokeza kumuaga Rais Kagame ambao wengi wao walikuwa ni wanawake na kuwatakia ‘heri ya Siku ya Wanawake’ ambayo huadhimishwa tarehe 08 Machi, kila mwaka duniani kote.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli amewashukuru wanawake wote hapa nchini kwa mchango wao mkubwa kwa Taifa na amesema Serikali inatambua na kuthamini juhudi zao mbalimbali.
“Mungu awabariki sana akina Mama, mnafanya kazi nzuri kwa ajili ya Taifa hili, endeleeni kuimarisha umoja wa Watanzania wote, Serikali ninayoiongoza inathamini sana kazi nzuri zinazofanywa na akina Mama, endeleeni kutembea kifua mbele, Mungu atawalinda, na mimi sasa hivi naondoka kwenda kumuona Mama yangu hospitalini katika siku yake hii, pia natoa shukrani nyingi kwenu na kwa viongozi wa Mkoa na Wilaya kwa jinsi mnavyojitolea kuwapokea na kuwaaga vizuri wageni wetu” amesema Rais Magufuli