Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameungana na watanzania katika janga la tetemeko la ardhi lililotokea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na kusababisha vifo vya watu 16 Bukoba Mjini.

Kupitia salamu zake za rambirambi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, Rais Kenyatta ameeleza kuguswa na maafa hayo na kuahidi kushikana mkono katika kipindi hiki kigumu.

“Kwa niaba yangu binafsi na Serikali ya Kenya, natuma salamu zangu za dhati za rambirambi kwako, Serikali na watu wa Tanzania na hasa familia za waathirika,” ilieza sehemu ya salamu hizo kwa Rais Magufuli.

Gazeti la Kenya la Daily Nation limeeleza kuwa Rais Kenyatta alimpigia simu Rais Magufuli na aliahidi kutoa misaada yake kwa waathirika ambapo leo ndege ya Jeshi la ulinzi la Kenya itawasilisha misaada mbalimbali nchini.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, jana aliwasili mjini Bukoba kuwatembelea waathirika na kutoa mkono wa pole kwa kaya 16 za waliofikwa na misiba kutokana na tetemeko hilo la ardhi.

Mbowe alitoa shilingi milioni 2.1 kwa ajili ya kaya hizo, mifuko 150 ya sementi kwa familia 15 ambazo zimepoteza makazi ambapo kila kaya ilipata mifuko 10.

Mwenyekiti huyo wa Chadema aliambatana na viongozi wengine wa  Chadema mjini humo pamoja na Mbunge wa Bukoba Mjini, Willfredy Rwakatale na Mbunge wa viti maalum (CUF), Saverina Mwijage, walitoa sukari sukari kilo 25 pamoja na mchele kilo 50.

“Ndugu zangu, tukio hili sio la Serikali au chama chochote, ni jambo la kitaifa. Serikali inapaswa kutenga fungu kubwa kwa ajili ya kuisaidia jamii,” Mbowe anakaririwa.

Akiwa katika shule ya Sekondari ya Ihungo iliyobomolewa na tetemeko la ardhi na kusababisha wanafunzi kukosa madarasa ya kusomea, Mbowe ambaye pia alisoma katika shule hiyo alitoa misaada mbalimbali.

Rais John Magufuli alilazimika kuahirisha safari yake ya kuhudhuria kuapishwa kwa Rais wa Zambia, Edgar Lungu kutokana na janga la tetemeko la ardhi, badala yake alimtuma Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kumuwakilisha.

Video: Omary Mtanzania anayeimba Taarabu Canada, asimulia mziki huo unavyokubalika Canada
Waiba Mashine za kupima tetemeko la ardhi