Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete jana aliitumia siku ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere kuwataka wananchi kulinda amani na umoja wa nchi huku akiwatahadharisha kutokiuka maagizo ya NEC ya kutobaki katika vituo vya kupigia kura baada ya kupiga kura, Oktoba 25.

Katika hotuba yake kwa taifa akiwa mjini Dodoma katika sherehe za maadhimisho ya Kumbukumbu za Mwalimu Julius Nyerere zilizoambatana na kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, rais Kikwete aliwataka wananchi kutowasikiliza viongozi wa vyama vya siasa wanaowataka kubaki katika vituo vya kupigia kura baada ya zoezi hilo.

Alisema watu watakaokiuka amri ya kutobaki katika eneo la vituo vya kupigia kura kwa lengo la kulinda kura hawatavumiliwa.

“Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wametoa matamko kuwataka wanachama wao wawahi kupiga kura Oktoba 25 mwaka huu halafu wakabaki kituoni kwa ajili ya kulinda kura. Mtu yoyote atayebaki kituoni kulinda kura atachukuliwa hatua za kisheria, msiilazimishe serikali kufanya yale yasiyopendeza, lakini ikibidi tutatimiza wajibu wetu,” alisema.

Kwa upande wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, baada ya kusikia kauli hiyo, aliendelea kuwahamasisha wafuasi wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, kulinda kura baada kupiga kura na kukaa umbali ambao sheria imeelekeza.

Hii ni sehemu ya tamko la Mbowe:

“Rais Kikwete amesema wananchi wakipiga kura waondoke vituoni na kwenda nyumbani na wasiofanya hivyo watashughulikiwa na vyombo vya dola. Nchi inaongozwa na sheria na Katiba si mapenzi ya Kikwete wala mtu yoyote. Kama Kikwete amezoea kuvunja katiba ya CCM, Watanzania hatutamruhusu avunje Katiba ya nchi, kwa sababu sheria ya Uchaguzi inasema siku ya kupiga kura, ukishapiga kura usikae chini ya mita 200 kutoka kituoni.

“Sheria inasema kukaa mita 200 ruksa, kwa sababu wanapanga kuiba krua, kuingiza kura feki wanataka Watanzania mkimbie kituo wakati kuna kura zetu, nasema tarehe 25 ni siku ya Kihistoria, tunaenda kubadili historia.

“Piga kura, hesabu mita 200 weka kambi mpango ndio huo hakuna woga.”

 

JK: Taifa Stars Ina Mlima Wa Kupanda
Magufuli: Marehemu Dkt Kigoda Alinishauri Dakika Za Mwisho