Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro amesema kuwa amefanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi lililoratibiwa na kiongozi wa upinzani, Juan Guaido.
Makumi ya wanajeshi ambao waliamua kumuunga mkono kiongozi huyo wa upinzani waliwasaidia waandamanaji kupambana na wanajeshi wanaomuunga mkono Rais maduro. Kwa mujibu wa BBC, watu 100 wameripotiwa kujeruhiwa.
Akizungumza kupitia kituo cha televisheni cha Taifa, Rais Maduro ameeleza kuwa jaribio la Guaido kutaka kulibadili jeshi limpinge limeshindwa.
Kwa upande wa Guaido, amesisitiza kuwa Rais Maduro ameshindwa kupata udhibiti wa majeshi yake huku akiendelea kuwahamasisha waandamanaji kurejea mitaani leo. Guaido anaungwa mkono na mataifa 50 ikiwa ni pamoja na Uingereza, Marekani na Latin America.
Leo, Marekani imeahidi kumpa Guaido msaada wowote ikiwezekana wa kijeshi. Hata hivyo, inakuwa upande wa Maduro unaungwa mkono pia na mataifa yenye nguvu kama Urusi na China na uongozi wote wa juu wa jeshi la nchi hiyo umekuwa mtiifu kwake.
Rais Maduro amewashutumu waandamanaji kwa kile alichoeleza kuwa wanafanya makosa makubwa ambayo hayawezi kupita bila adhabu wanayostahili.
Mahasimu hao wawili wameendelea kuwahamasisha wafuasi wao kuingia barabarani hali inayotishia amani na utulivu katika taifa hilo ambalo linakabiliwa na changamoto ya kiuchumi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amedai kuwa Serikali ya Guaido imeandaa ndege maalum kwa lengo la kumkimbiza nchini Cuba na kwamba walipanga kufanya hivyo Jumanne wiki hii. Hata hivyo, Guaido amekanusha vikali madai hayo na kueleza kuwa propaganda za Marekani za kutaka kumuondoa zitaendelea kushindwa.