Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameivunja Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa) kuanzia leo.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu iliyotolewa leo Jumapili Septemba 23,2018, imesema Rais Magufuli amechukua hatua hiyo baada ya kutokea kwa ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere.
Amesema bodi hiyo iliyo chini ya mwenyekiti wake Brigedia Jenerali Mstaafu Mhandisi Mabula Mashauri imevunjwa kuanzia leo wakati kamati ya uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea na uchunguzi wa ajali hiyo.
Rais Magufuli ametangaza kuivunja bodi ya Tamesa ikiwa ni siku tatu zimepita tangu kutokea kwa ajali ya Kivuko cha MV Nyerere.
Akitoa taarifa za ajali hiyo leo Septemba 23, 2018, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema licha ya kivuko hicho kuwa na uwezo wa kubeba abiria 101 siku ya ajali kilikuwa kimebeba abiria 265.
Waziri Kamwelwe amesema hayo mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika shughuli ya mazishi katika eneo la Shule ya Sekondari Bwisya.
Pia ametoa mchanganuo wa vifo, ambapo ameeleza kuwa wanawake 126, wanaume 71, watoto wa kike 17, watoto wa kiume 10 na kufanya jumla ya maiti 224.
Amesema miili 219 iliyotambuliwa yote ilichukuliwa na kwenda kuzikwa na ndugu zao, wanne walikuwa hawajatambuliwa na wamechukuliwa vipimo vya DNA ili ndugu zao watakapofika waweze kutambua kuwa wamepoteza ndugu.
“Miili mingine mitano iliyotambuliwa ndugu zao waliamua kuungana nasi katika mazishi haya lakini kuna huyo mmoja tuliyempata sasa hivi taratibu zitaendelea baadaye,” amesema Kamwelwe.
Amesema ajali ilitokea Septemba 20, 2018 saa 7:48 mchana na saa 8:10 mchana taarifa zilifika kwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella aliyekuwa katika kikao cha ulinzi na usalama na saa 10 jioni yeye na kamati hiyo waliwasili eneo la tukio na kukuta wananchi tayari wameokoa watu 40.
Idadi ya 265 inatokana na waliofariki kuwa 224 na waliookolewa 41. Hata hivyo, shughuli za uokoaji zinaendelea.
Kuhusu michango inayotolewa, amesema, “Mpaka sasa pesa zilizochangwa na wananchi ni Sh190 milioni ili kusaidia katika shughuli hizi.”
“Mbali na hilo Serikali pia iko katika mpango wa kununua vivuko salama ili wananchi waweze kuendelea na shughuli za kiuchumi,” ameongeza.