Rais John Magufuli amekumbushia jinsi ambavyo msimamo na uimara wa rais mstaafu, Jakaya Kikwete ulivyomuwezesha kuingia Ikulu mwaka 2015.
Akizungumza jana Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya ufunguzi wa taasisi ya Jakaya Kikwete, Rais Magufuli alisema kuwa hataacha kumshukuru kila wakati wanapokutana bila kujali.
“Kwako Kikwete napenda kukuahidi kuwa nitaendelea kukushukuru kila tutakapokutana, ukichukia, ukifurahi mimi nitakushukuru kwa sababu wewe ndiye uliyesimama imara mpaka leo hii mimi ni Rais,” alisema rais Magufuli.
Aidha, alitambua mchango wa Kikwete katika kuleta maendeleo ikiwa ni pamoja na ubora wa miundombinu uliofanyika wakati wa akiwa rais. Alisema rais huyo mstaafu katika awamu yake alifanya mengi ikiwa ni pamoja na kujenga shule za kata, barabara na hospitali.
Alipongeza pia uanzishwaji wa taasisi ya Jakaya Kikwete ambayo imejikita katika masuala ya afya, vijana na utawala bora. Rais Magufuli aliahidi kuwa serikali yake itaiunga mkono taasisi hiyo kwani ina tija katika sekta zote inazohusika nazo.
- Lowassa ajibu mapigo, ‘mimi kupima DNA ni upuuzi’
- Video: Rais Dkt. Magufuli azindua Taasisi ya Jakaya Kikwete
Akizungumzia taasisi yake, Kikwete alisema kuwa pamoja na mambo mengine, imelenga kuwasaidia vijana kuwapa mafunzo ili wawe na elimu, wazalendo na wenye maadili mema wakitumia akili na nguvu zao kujiletea maendeleo.