Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, leo Machi 3, 2020 amekutana na kufanya mazungumzo na wenyeviti wa vyama vya siasa vya upinzani, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na mshauri wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Maalim Seif amesema kuwa yeye na Rais Magufuli wamezungumzia umuhimu wa kudumisha amani, umoja na usalama wa Tanzania, na mazungumzo yao yameenda vizuri.
“Mimi na Mheshimiwa Rais tumekutana na kubwa tumezungumzia mambo ya nchi yetu. Ni vipi tutaendelea kuifanya Tanzania kuwa nchi ya amani, nchi ya usalama, nchi ya upendo kwa Watanzania wote, ndio kiini cha mazungumzo yetu,” alisema Maalim Seif.
Akimzungumzia Rais Magufuli, alisema ni mtu muwazi na anayejali na kukubali kukutana na wananchi wake.
“Mimi namshukuru Rais kwamba amekubali tukutane na tuzungumze kwa maslahi ya nchi yetu. Namshukuru sana, sasa kuna mengine tumezungumza mimi na Rais, kwa sababu yale yamo ndani huwezi kuyataja hapa na bila shaka kukiwa na haja ya kukutana tutakutana,” aliongeza.
Kwa upande wa Profesa Lipumba, yeye alieleza kuwa anashukuru Rais Magufuli ameahidi kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa huru na haki. Hivyo, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza na kushiriki kuwachagua viongozi wanaowapenda. Mwenyekiti huyo wa CUF amepongeza juhudi za Serikali ya Rais Magufuli katika kupambana na rushwa na kuimarisha uchumi.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi amewataka wanasiasa wenzake kufanya siasa za kistaarabu na kuepuka mambo yanayoweza kuchochea migongano na kukamiana. Amewataka kuipongeza na kuiunga mkono serikali katika mambo inayofanya vizuri kama elimu na nishati.
Viongozi hao wamezingatia ushauri wa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wa kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono au kukumbatiana, wamesalimiana kwa njia mbadala za kuoneshana mikono na kugonga miguu.