Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameongoza mamilioni ya Watanzania kutuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwenyekiti wa makampuni ya IPP na moja ya watu matajiri na mashuhuri nchini Tanzania Reginald Mengi.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter Rais Magufuli amesema ataendelea kumkumbuka Mzee Mengi kwa mchango wake katika maendeleo ya taifa.
“Nimesikitishwa na taarifa za kifo cha Mzee na Rafiki yangu Dkt. Reginald Mengi. Nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu na maono yake yaliyopo katika kitabu chake cha I Can, I Will, I Must. Poleni wanafamilia, wafanyakazi wa IPP na Jumuiya ya Wafanyabiashara” Ameandika Rais Magufuli.
Naye Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dkt Hassan Abbas ameeleza kupokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mzee Reginald Mengi.
“Kama alivyopata kusema yeye mwenyewe siku za uhai wake kuwa watu wanaoacha alama hawafi, basi mawazo, falsafa, ubunifu na kujitoa kwake vitaendelea kuishi nasi, R.I.P Mzee Mengi.” Amesema Dkt. Abbas.
Mzee Mengi alizaliwa mwaka 1944 mkoani Kilimanjaro na umauti umemkuta akiwa mjini Dubai, Falme za Kiarabu baada ya kuugua kwa muda mfupi, kwa mujibu wa familia yake.