Rais John Magufuli amempongeza aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila kwa kuibua bungeni sakata la Tegeta Escrow lililoiweka matatani kampuni ya kufua umeme ya IPTL na baadhi ya vigogo Serikalini.
Rais Magufuli ametoa pongezi hizo kwa Kafulila alipokuwa akiwahutubia wananchi wa wilaya Uvinza mkoani Kigoma katika sehemu ya ziara yake kusini mwa Tanzania ambapo ameeleza kuwa waliombeza na kumuita mwanasiasa huyo tumbili wao ndio tumbili.
“Napenda kumpongeza Kafulila ambaye alijitoa na kuibua sakata la IPTL, wengine walimuita tumbili kwa kumbeza sasa wao ndio watakuwa tumbili,” Rais Magufuli alisema.
“Aliyemuita Kafulila tumbili yeye ndiye tumbili, Kafulila katetee wanyonge hadi wakudhihaki ila wao ndio tumbili, wewe ni mtu safi,” aliongeza.
- Israel, Palestina kwachafuka, Mahmoud Abbas akata mawasiliano
- Magazeti ya Tanzania leo Julai 23, 2017
Pongezi za Rais Magufuli kwa Kafulila zinawakumbusha Watanzania jinsi ambavyo alipata pingamizi kubwa na mtafaruku alipoibua sakala la Tegeta Escrow bungeni mwaka 2014, ambapo aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema alimpinga vikali na kumuita ‘tumbili’.
Hata hivyo, busara za aliyekuwa mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu ziliepusha vurugu zilizoibuka bungeni kuhusu sakaka hilo kati ya wawili hao, lakini siku chache baadae Bunge liliunda tume maalum ikiongozwa na Zitto Kabwe.
Tume hiyo iliwasha moto zaidi kwenye sakata hilo na kupelekea mawaziri waliotajwa kwenye sakata hilo wakidaiwa kupokea mgao kutoka kwa mkurugenzi wa kampuni ya VIP Engineering ambaye pia ni mmiliki mwenza wa kampuni ya IPTL, James Rugemarila. Jaji Werema pia alijiuzulu kutokana na sakata hilo.
Kafulila aliwashukia aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Jaji Werema kwa madai kuwa walisema uongo kuhusu uamuzi wa kutoa fedha kwenye akaunti maalum ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu, na kuipa kampuni ya IPTL wakati kesi ya usuluhishi kati ya IPTL na Tanesco ikiwa inaendelea.
Hivi karibuni, ikiwa imepita takribani miaka mitatu tangu kuibuliwa kwa sakata hilo, Serikali imewafungulia kesi ya uhujumu uchumi mmiliki wa IPTL, Rugemarila na mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya PAP, Habinder Seth Sigh.
Wawili hao bado wako mahabusu kwani mashtaka dhidi yao hayaruhusu dhamana na kesi dhidi yao inaendelea.