Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt Mwigulu Nchemba kufanya uchunguzi kuhusu umakini katika Maabara Kuu ya Taifa iliyopewa jukumu la kupima virusi vya corona kutokana na kuwepo kwa utata katika majibu ya sampuli mbalimbali.
Rais Magufuli amesema sampuli mbalimbali zilipelekwa katika maabara hiyo ikiwa ni pamoja na zile za kutoka kwa mbuzi, kondoo, papai na fenesi na majibu yameonyesha baadhi ya vitu hivyo vina maambukizi ya corona.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Mei 3, 2020 akiwa Chato mkoani Geita wakati wa hafla ya kumuapisha Dkt. Nchemba wilayani na kuongeza kuwa uchunguzi uliofanywa umebaini sampuli mbalimbali zisizo za binadamu zilizopelekwa katika maabara hiyo kutoa majibu yanayoonesha zina maambukizi ya virusi vya corona.
Aidha, amemuagiza Waziri Nchemba kushirikiana na wataalamu wa Wizara katika kuhakiki umakini wa vifaa vilivyopo katika maabara hiyo pamoja na uwezo wa wataalamu waliopo kwa ajili ya kufanya kazi ya upimaji.
Hivi karibuni Rais Magufuli, alikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini na kuwaagiza kuchunguza utendaji kazi wa vipimo hivyo na kuchukua sampuli hizo ambazo baadhi majibu yameonesha kuwa na utata.