Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amemteua Rais mstaafu awamu ya pili, Alhaji Hassan Mwinyi kuwa mdhamini wa skauti nchini katika hafla ya uapishaji wa viongozi uliofanyika leo ikulu jijini Dar es salaam.
“Nikupongeze mzee wangu, kwani umekuwa mzee asiyetaka makuu na haukusita katika uteuzi niliokupa, na nina jua utakayokuja kunieleza yatakuwa ni amri na sio ombi, na lazima nitayatekeleza” amesema Magufuli.
Katika hotuba yake Dkt Magufuli amewapongeza viongozi wateule na kuwataka washirikiane na viongozi wenzao katika ufanyaji kazi kwa uweredi ili kuleta mabadiliko chanya ndani ya serikali na Tanzania kwa ujumla. Huku akimshukuru Ally Hassan Mwinyi kwa kuitikia ombi lake.
Viongozi walioapishwa ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt Faraji Mnyepe na Mkuu wa Skauti nchini, Bi Mwantumu Bakari Mahiza.
Niwapongeze Skauti wote nchini kwa kufanya kazi nzuri, Mama Mahiza umeshika nyadhifa mbalimbali katika taifa hili,ninajua sijafanya makosa kukuteua umekuwa mahiri na shujaa na nina hakika kazi itaenda mbele” Amesema Magufuli.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Dkt Mnyepe amesema kati ya mambo atakayoyapa kipaumbele ni pamoja na masuala ya ujibuji wa barua ndani ya Wizara pamoja na waraka wa rais wa mwaka 1964 ambao unajenga utaratibu wa ufanyaji kazi baina ya wizara na mabalozi mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Naye Bi Mahiza amemuahidi Dkt Magufuli kueneza skauti katika vyuo vya kati na vyuo vikuu hapa nchini pamoja na kufanikisha ujenzi wa kambi ya kimataifa mkoani Dodoma, huku akipongeza juhudi zinazofanywa na chama hicho ndani na nje ya nchi.