Rais John Magufuli amempa neema ya ukwasi, mzee Jumanne Ngoma, aliyegundua madini ya Tanzanite katika maeneo ya Merarani.
Akihutubia leo wakati wa uzinduzi wa ukuta wa mgodi huo, Rais Magufuli amesema kuwa Serikali imempa mzee huyo kiasi cha shilingi milioni 100, kwa kuthamini mchango wake.
Alisema kiasi hicho kitamsaidia pia mzee Ngoma ambaye alihudhuria uzinduzi huo, kugharamia matibabu yake kwani amepooza miguu.
“Watu hawa hawatambuliwi, angalia mzee huyu aliyegundua madini haya. Leo tusingekuwa hapa kama asingekuwa huyu mzee. Angalia sasa amepooza mguu wake,” alisema Rais Magufuli.
Mzee Ngoma alifika katika uzinduzi huo na kupelekwa mbele kwa agizo la Rais akiwa ameshikiliwa kutokana na ugonjwa unaomkabili.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alionesha kuwashangaa watu walikuwa wakifurahia kushikiliwa kwa ndege ya Tanzania nchini Canada akifananisha kitendo hicho na ‘ushetani’.
Rais Magufuli leo amezindua ukuta unaozunguka mgodi wa madini ya Tanzanite uliojengwa na jeshi.