Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amemrejesha Bungeni, Anne Kilango Malecela kupitia mamlaka aliyonayo kisheria ya kuteua wabunge.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, Anne Malecela ataapishwa kwa mujibu wa taratibu za Bunge. Hii inamaanisha katika vikao vijavyo vya Bunge.
Malecela ambaye awali alikuwa Mbunge wa Same Mashariki kwa kipindi cha miaka kumi (2005-2010) anarejea Bungeni ikiwa ni miezi takribani 9 tangu Rais Magufuli alipotengua uteuzi wake wa Ukuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa sababu za kutoa taarifa za uongo kuhusu uwepo wa watumishi hewa mkoani kwake.
Malecela alikuwa muathirika wa oparesheni ‘tumbua majipu’ inayoendeshwa na Serikali ya Awamu ya Tano, muda mfupi baada ya kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa hakuna mfanyakazi hewa hatammoja mkoani kwake. Tume maalum ya Rais ilibaini uwepo wa rundo la wafanyakazi hewa mkoani humo muda mfupi baadae.
Mbali na kuwa mbunge machachari wa CCM ndani ya Bunge kwa namna alivyojenga hoja, Malecela aliwahi kushika nafasi ya Unaibu Waziri wa Elimu katika kipindi cha mwisho cha Serikali ya Awamu ya Nne iliyoongozwa na Dkt. Jakaya Kikwete.