Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo, Novemba 3, 2019 amemteua Charles Kichere kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akichukua nafasi ya Profesa Mussa Assad.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Rais Magufuli amefanya uteuzi huo leo kwakuwa muda wa Profesa Assad kuwa CAG unakwisha kesho, hivyo Kichere anaanza rasmi kazi kesho.
Kichere aliwahi kuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na baadaye uteuzi wake ulitengulia. Rais Magufuli alimteua tena kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, na sasa atakuwa CAG.
Aidha, Balozi Kijazi ameeleza kuwa nafasi ya Ukatibu Tawala wa Mkoa wa Njombe imejazwa na Katarina Revocati. Awali, Bi. Revocati alikuwa Msajili Mkuu wa Mahakama.
Katika taaria hiyo, Balozi Kijazi ameeleza kuwa Rais Magufuli amemteua Aisha Amour kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait.
Wengine walioteuliwa leo ni pamoja na Kanali Francis Mbindi anayekuwa Kamishna wa Kazi Ofisi ya Waziri Mkuu.
Rais Magufuli pia amefanya uteuzi wa Majaji kumi na wawili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.