Leo Agosti 1, 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemuapisha Benedict Martin Mashiba kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi.
Rais Magufuli amemuapisha balozi huyo mpya kuchukua nafasi ya Victoria Richard Mwakasege ambaye amestaafu.
Pia, Rais Magufuli amepokea hati za utambulisho wa Mabalozi watano walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Akizungumza na mabalozi hao, amewapongeza mabalozi hao kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na nchi hizo ambazo ni marafiki wa muda mrefu na washirika wa maendeleo wa Tanzania.
Aidha, Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kutilia mkazo diplomasia ya uchumi kwa kuongeza juhudi za kuhamasisha wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo wa nchi hizo kushirikiana na Tanzania katika biashara na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda, kilimo na huduma za kijamii.
Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho wamemshukuru Rais Magufuli kwa kuwapokea na wameahidi kuhakikisha uhusiano wa nchi zao na Tanzania unaendelezwa na kuimarishwa zaidi.
Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho ni;
1. Nguyen Kim Doahn – Balozi waVietnam hapa nchini.
2. Prof. Ratlan Pardede – Balozi waIndonesia hapa nchini.
3. Mwadhama Askofu Mkuu Marek Solcynski–Balozi waVaticanhapa nchini.
4. Dkt. Detlef Wachter – Balozi waUjerumani hapa nchini.
5. Richard Tumisiime Kabonero – Balozi waUganda hapa nchini.