Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameombwa kuvifutia vyombo vya habari vya dini leseni za uendeshaji kibiashara na badala yake kuwaweka katika mfumo usio wa kibiashara.
Ombi hilo limetolewa na Askofu wa Kanisa la Agape, Vernon Fernandes mapema leo Januari 23, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam katika kikao kati ya Rais John Magufuli na viongozi wa dini ili kuzungumza masuala yanayohusu nchi.
Askofu Fernandes amesema “TCRA wameifuta Non Commercial License wanataka sisi tufanye kazi kama ITV, EATV, tutawezaje kulipa leseni ya kibiashara wakati hatuna matangazo yanayoweza kutuingizia pesa hizo zinazotakiwa,”
Kwa upande mwingine, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Amani Lyimo amemuomba Rais Magufuli kuwaachia uhuru wananchi wazungumzie inapowezekana kwa sababu hiyo ndiyo demokrasia.
Mchungaji Lyimo amesema katika mkutano huo kati ya Rais Magufuli na viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini.
Amesema Watanzania wengi wanahofu hata kama haambiwi na watendaji wake ila wengi hawathubutu kuzungumza licha ya kuwa anafanya mambo mengi mazuri.
“Kwa kazi unayoifanya watu hawatachagua maneno bali watachagua kazi, kwa hiyo kama kuna uwezekano waachie pumzi kidogo wazungumze lakini hawatakushinda kwa maneno yao,” amesema Lyimo.