Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesifu mkakati wa mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi wa kusimamia kodi zinazotokana na mazao ya misitu kuwa mkoa umefanya vizuri Sana anaripoti mwandishi wetu Francis Godwin toka Iringa
Rais Dkt Magufuli ametoa pongezi hizo wakati akiwasalimia wananchi wa mji wa Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa akiwa ziarani mkoani humo.
Akijibu ombi la mbunge wa jimbo la Mafinga mjini Cosato Chumi aliyeomba malori kuruhusiwa kutembea mchana,Rais Dkt Magufuli alisema kuwa uamuzi wa malori mazao ya misitu kuzuiwa kutembea usiku ulilenga kuthibiti ajali za barabarani hivyo kama madereva hawataweza kusababisha ajali sheria hiyo inaweza kurekebishwa
Kuhusu suala la nguzo za umeme waziri Dkt Magufuli aliiagiza waziri kuwaagiza watekelezaji wa miradi ya umeme nchini kuacha kununua nguzo za umeme kwa kampuni ya Saohili tu ambayo ni ya serikali na badala yake kununua nguzo hizo kwa watu binafsi wenye uwezo wa kutengeneza nguzo hizo.
Aidha, Rais Dkt Magufuli alikubali ombi la mbunge Chumi la kuruhusu majengo yaliyokuwa yakitumiwa na wajenzi wa barabara ya Mafinga-Makambako kutumika kwa ajili ya shughuli za kijamii wilaya ya Mufindi.
Alimtaka Meneja wa wakala wa barabara mkoa wa Iringa -TANROADS kuyakabidhi majengo hayo kutumika kwa shughuli nyingine.
Akiwa katika eneo la Nyololo jimbo la Mufindi kusini Rais Dkt. Magufuli alisema Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara kutokana na bajeti ya nchi kwani suala la kupanga ni kuchagua.
Alisema Serikaki itaendelea kuboresha miundo mbinu na kushughulikia kero mbali mbali za wananchi kulingana na ilani ya CCM ilivyoagiza.
Mkoa wa Iringa toka umefanikiwa kukusanya kodi zitokanazo na mazao ya misitu kwa muda wa miezi mitatu jumla ya zaidi ya Shilingi bilioni 3.4
Ukusanyaji wa kodi hiyo ambayo awali ilikuwa inakwepwa na wafanyabiashara wa nguzo umetokana na jitihada za uongozi wa mkoa wa Iringa chini ya mkuu wa mkoa Hapi na timu yake ambaye alizuia nguzo kutoka Iringa bila kutoa ushuru stahiki na sio asilimia 5 kwa nguzo kama walivyokuwa wakitozwa na halmashauri.
Wakati huo huo Rais Dkt. Magufuli amelazimika kusimama kijiji cha Ifunda jimbo la Kalenga kuwasalimia wananchi waliokuwa wamesimama barabarani kumsubiri pamoja na mvua kubwa kuendelea kunyesha.