Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesimamisha zoezi la kubomoa makazi ya watu waliojenga bila kufuata taratibu za mpango mji.
Rais Magufuli amesema kuwa nyumba hizo zisibomolewe kwa kuwa hayakuwa makosa yao kujenga katika maeneo hayo na kuelekeza kuwa watu wote wasio na hati miliki za ardhi kufanyiwa urasimishaji wa makazi yao.
“Serikali ya awamu ya tano kuanzia sasa haitabomoa tena nyumba za wananchi waliojenga maeneo ya makazi yasiyo rasmi badala yake itarasimisha makazi holela,” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo na Makazi, William Lukuvi akiwa wilayani Simanjiro mkoani Manyara akifanya ziara yake ya kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi kwa wakazi wa mji huo amewataka wananchi wote wachangamkie fursa hiyo iliyotolewa na Rais.
“Serikali ya awamu ya tano inajali sana wananchi wake kwakuwa zamani wananchi ambao hawakujenga kwa kufuata mipango miji wangebomolewa nyumba zao, lakini kwa sasa imeanzisha mpango kurasimisha makazi holela na kuwapatia hati wananchi wote waishio mijini ili waishi katika makazi rasmi,” amesema Lukuvi.
Pamoja na hayo Lukuvi amewataka wananchi wote waishio mijini kuwa wazalendo kwa kurasimisha maeneo yao waweze kujipatia hati na ili walipe kodi ya pango la ardhi jambo ambalo litaiongezea Serikali mapato