Rais John Pombe Magufuli amefanya uteuzi katika nafasi za ukatibu mkuu na Mganga Mkuu wa Serikali, uteuzi ambao unaanza rasmi leo, Aprili 22, 2020.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Rais Magufuli amemteua Dkt. Zainab Abdi Chaula kuwa Katibu Mkuu wa Mawasiliano, akichukua nafasi ya Dkt. Maria Sasato ambaye amestaafu.
Kabla ya uteuzi huo Dkt. Chaula alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Aidha, Rais Magufuli amemteua Profesa Mabula Daudi Mchembe kuwa katibu mkuu wa wizara hiyo inayoshughulikia afya. Kabla ya uteuzi huo, Profesa Mabula alikuwa msaidizi wa Rais katika masuala ya afya.
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa Rais Magufuli amemteua Profesa Abel Makubi kuwa Mganga Mkuu wa Serikali akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Mohamed Bakari Kambi ambaye amestaafu
Kabla ya uteuzi huo, Profesa Makubi alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.