Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu 14 waliopoteza maisha baada ya basi dogo walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori la kubebea mchanga katika eneo la Dundani Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Ajali hiyo imetokea mapema leo Juni 25, 2018 wakati basi dogo lililowabeba wanafamilia, ndugu na jamaa waliokuwa wakielekea Msata kuhudhuria sherehe za kumaliza mafunzo ya kijeshi kwa mtoto wao, kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa linatoka Dar es salaam kwenda Dundani kuchukua mchanga.
Kufuatila taarifa hiyo, Rais Magufuli ametoa salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ambapo ameeleza kusikitishwa kwake na ajali hiyo mbaya iliyozima maisha ya watanzania 14.
“Naomba unifikishie pole nyingi kwa wanafamilia wote waliopatwa na msiba, waambie naungana nao katika kipindi hiki kigumu cha majozi ya kuondokewa na wapendwa wao, na sote tuwaombee Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewaombea majeruhi wa 4 wa ajali hiyo wapone haraka ili waweze kuungana na familia zao na kuendelea na majukumu yao ya kila siku.