Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi na pole kutokana na ajali ya kivuko cha Mv. Nyerere kilichozama Septemba 20, 2018 huku watu 37 mpaka sasa wakiripotiwa kufariki dunia.
Kivuko hicho kilikuwa kinatoka Bugorora kwenda Ukara katika Ziwa Victoria kimezama kikidaiwa kuwa na watu zaidi ya 100.
Rais Magufuli ametoa salamu hizo kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Gerson Msigwa aliyepiga simu Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wakati wa taarifa ya habari.
“Rais anatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki waliofikwa na ajali,” amesema Msigwa
Msigwa amesema, “Rais anaomba Watanzania kuwa watulivu wakati juhudi za uokoaji zinaendelea na baadaye Serikali itaweza kutoa taarifa cha nini kitakachoendelea.”
Msigwa amesema taarifa ambazo Rais Magufuli amezipata kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela zinasema, Kwamba zaidi ya watu 40 wameokolewa.”
Hata hivyo, kabla ya Msigwa kupiga simu, watangazaji wa habari wa TBC wamesema miili ya watu kumi ilikuwa imepatikana na 44 walikuwa wameokolea huku Mkuu wa mkoa huo akiwa ametangaza kusitisha shughuli ya uokoaji.
Mmoja wa mashuhuda waliohojiwa na TBC, Lazaro Mgusi amesema, “Ni kawaida siku za Alhamisi kivuko hicho kujaza kutokana na kuwepo kwa gulio.”
Lazaro ameiomba Serikali kukiboresha kwani kimekuwa kikibeba watu.
Naye, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna amesema hadi sasa waliofariki dunia ni 37, kwamba ukoaji jana ulisitishwa hadi leo asubuhi.