Rais John Magufuli amevionya vyombo vya habari nchini akivitaka kujiepusha na habari za uchochezi bali vijikite katika habari za maendeleo kwa ajili ya Taifa.
Akizungumza leo baada ya kuwaapisha Mabalozi na Mawaziri aliowateua hivi karibuni, Rais Magufuli amesema kuwa kumekuwa na tabia ya waandishi wa habari kujikita zaidi katika kuandika habari zenye mlengo hasi zaidi na kuzipa nafasi kubwa huku wakizifumbia macho habari za maendeleo.
“Unakuta kwenye TV fulani hivi, kila wakulima au wafugaji wanapoandamana ndio heading (kicha cha habari) na inachukua muda mrefu sana. Hiyo ndiyo stori kwao. Kila kitu chenye uchochezi fulani fulani kwao ndio stori. Sasa Mwakyembe kafanye kazi. Kama waliokuwepo waliokuwa wanashindwa kuchukua hatua wewe kachukue,” alisema Rais Magufuli.
Alitoa mfano wa magazeti ya hivi karibuni ambapo alieleza kuwa baadhi ya magazeti yaliweka habari fulani kwenye kurasa zaidi ya moja, kwa lengo la kuonesha kosa alilofanya mtu mmoja kama vile limefanywa au kuungwa mkono na Serikali.
Aidha, Rais Magufuli aliwaonya wamiliki wa vyombo vya habari akiwataka kuwa makini na kuangalia mienendo ya vyombo vyao.
“Nawaambia wamiliki wa vyombo vya habari, be careful. Watch it. Kama mnafikiri mna freedom ya namna hiyo not to that extent (sio kwa kiwango hicho),” aliongeza.
Alivitaka vyombo vinavyosimamia haki ikiwa ni pamoja na majaji waliohudhuria katika tukio hilo, kuhakisha wanaendeleza kazi nzuri wanayoifanya huku akiwahakikishia kuwa yuko pamoja nao wakati wote katika kuiendeleza Tanzania.