Rais Dkt John Pombe Magufuli amewataka wakurugenzi watendaji wateule 185 wa majiji, manispaa, miji na halmashauri za wilaya wawe ni watatuzi wa kero za wananchi badala ya kuwa watengeneza kero na akasisitiza wawe mitume wazuri kwa wananchi.

“Kaondoeni kero kwa wananchi wa hali ya chini, wako huko wanatozwa kodi ndogondogo hata za kuuza mchicha tu. Mtu akivuna mpunga wa kula nyumbani kwake pia anatozwa kodi, ni lazima kodi hizi mkazizuie kwa sababu tuliahidi kupunguza kero kwa wananchi na siyo kuongeza kero kwao,” – alisema.

Rais Magufuli amesema ana imani nao kwamba wataenda kutekeleza ilani ya CCM na akawataka waandae mipango yao ya maendeleo kila mmoja kulingana na eneo alilopo, waitekeleze hiyo mipango, na wafanye kazi kwa kushirikiana na viongozi walio juu yao na walio chini yao.

Amesema katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano, Serikali imedhamiria kujenga Tanzania yenye uchumi wa viwanda na kuwataka wasimamie kilimo ili mazao yatakayozalishwa yaweze kusindikwa hapa nchini. “Nendeni mkajipange tuwe na viwanda vidogo vidogo katika maeneo yenu”, alisisitiza.

“Nataka watu wafanye kazi. Bila kazi hakuna hela. Nataka mkahimizie tabia ya kufanya kazi ili kujiletea maendeleo yetu. Watanzania wote bila kujali dini zetu, vyama au makabila ni lazima tufanye kazi kwa sababu nataka Tanzania iingie haraka kwenye mataifa ya uchumi wa kati, na hili linawezekana,” alisema huku akishangiliwa.

Ndoa Ya TFF Na Azam Media Ltd Yaimarishwa
Waziri wa Afya Atumbuliwa, Rwanda