Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ametengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kutokana na sakata la kusainiwa kwa mkataba mbovu kati ya Jeshi la Zima Moto na Kampuni moja ya Romania; na bila kufuata sheria za nchi.
Akizungumza wakati wa kuzindua nyumba za maafisa na askari wa Jeshi la Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema kuwa Jeshi la Zima Moto walienda Ulaya na kusaini mkataba wa mkopo wa Euro milioni 408, wakati kisheria anayetakiwa kukopa fedha kwa ajili ya nchi ni Wizara ya Fedha na Mipango.
Pia, alisema kuwa mkataba huo ulisainiwa bila kupitishwa na Bunge na kwamba hata Watanzania waliohusika katika mchakato huo walikuwa wakilipwa kiasi kikubwa cha fedha kinyume cha utaratibu kama fedha za kujikimu wakiwa kwenye vikao nchini Romania.
“Palikuwa na mkataba wa ajabu unatengenezwa mambo ya ndani, wa zaidi ya Tril. 1 na umesainiwa na Kamishna Jenerali wa Fire, na haujapangwa na kupitishwa na Bunge, wakati wa vikao na kampuni moja kutoka Romania walipokuwa wakienda kwenye mkutano walilipana pesa nyingi,” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais amesema kuwa kutokana na sakata hilo, Kamishna wa Jeshi la Zimamoto, Thobias Andengenye pia hawezi kusalimika kwani alihusika katika kusaini mkataba huo bila kufuata taratibu na sheria za nchi.
Rais Magufuli amempongeza aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kwa kuchukua hatua na kuomba kujiuzulu. Amesema anampenda na anamheshimu lakini hana budi kukubaliana na barua yake ya kujiuzulu.
“Lugola ni Mwanafunzi wangu, nakupenda lakini kwenye hili hapana. Umenisifia hapa nakushukuru ila kwenye hili hapana,” amesema Rais Magufuli.
“Sitaki kuwa mnafiki. Andengenye unafanya vizuri, umejenga nyumba hadi Chato. Ila unaenda Ulaya unasaini Mradi hata Bunge halijapitisha, hapana,” aliongeza.
Rais Magufuli alisema kuwa hata yanayotakiwa kufanyika kutokana na mkataba huo ni mambo yasiyo na tija.
Julai Mosi, 2018 Lugola aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Mwigulu Nchemba.