Spika wa Bunge Mstaafu, Pius Msekwa amesema uteuzi wake wa kuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (MUST) uliofanywa na Rais John Magufuli Desemba 6 ,2018 haukuwa ni kwa makosa na kwamba Rais anatambua utendaji wake na uzoefu alionao kwa kuongoza baadhi ya vyuo vikuu nchini kikiwapo Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM).
Ameyasema hayo wakati akizungumza katika mahafali ya sita ya chuo hicho, ambapo amesema kupitia nafasi hiyo atahakikisha chuo hicho kinakuwa chachu ya kuzalisha wataalamu wa nyanja mbalimbali na kwamba amekuwa na bahati ya kuteuliwa kwa awamu ya tatu sasa kuongoza vyuo vikuu nchini.
“Kwanza kuna kila sababu ya kumshukuru Rais kwa kuniona mimi nafaa kuvaa kiatu hiki kwani kuna watu wengi serikalini lakini kaona mimi ndiye sahihi zaidi, nitaitumia fursa hii kuboresha elimu ya sayansi na teknolojia sambamba na kuongeza udahili kwa mwaka 2019/2020”, amesema Msekwa.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Zakia Meghji ameshauri uongozi wa chuo hicho kufanya tafiti katika nyanja mbalimba ili kuchochea maendeleo ya uchumi wa viwanda.