Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa ataanza kulifanyia kazi suala la nchi ya Zimbabwe kuhusiana na vikwazo ilivyowekewa na nchi za Magharibi.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam katika ukumbi wa Kimataifa wa Mkutano wa Julius Nyerere wakati akihutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Kusini mwa Afrika –SADC mara baada ya kukabidhiwa Uenyekiti wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo na Rais wa Namibia, Dkt. Hage Geingob.

Amesema kuwa sababu zilizosababisha nchi ya Zimbabwe kuwekewa vikwazo havipo tena, hivyo ni vyema Jumuiya ya Kimataifa ikaondoa vikwazo hivyo kwani vinawaumiza watu wasio na hatia.

“Naomba ndugu zangu wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika -SADC tuungane na kupaza sauti zetu, tuwe na kauli moja, tutamke kwa pamoja sasa vikwazo Zimbabwe basi,”amesema Rais Magufuli

Akielezea hali halisi ya uchumi na pato la Taifa moja moja kwa upande wa nchi wanachama, Rais Magufuli amesema kuwa sababu kubwa inayowafanya wawe na uchumi dumavu usiokua ni kwa sababu ya kuendelea kutegemea kuuza malighafi kwa nchi zilizoendelea.

“Ukiuza malighafi ujue unauza na nafasi za ajira za watu wako, ndio maana kwetu Barani Afrika na hususani Kusini mwa Jangwa la Sahara tuna tatizo kubwa kwa vijana wetu kupata ajira,”amesema JPM

Aidha, Rais Magufuli ameongeza kwa kusema kuwa utatuzi wa jambo hilo ni kuamua SADC kuwa nchi za Viwanda, kwa kuwa hakuna nchi yeyote duniani ambayo imeendelea bila ya kuwa na Viwanda.

Pia, Rais Magufuli amesisitiza kuwa ajenda yake kubwa kama Mwenyekiti wa SADC ni kuwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, ambayo itajikita na kuwekeza kwenye Viwanda, ili iweze kutoa nafasi ya kutimiza malengo ya jumuiya kama inavyosema kauli mbiu ya Mazingira Wezeshi kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu ya Viwanda, Ongezeko la Biashara na Ajira Kikanda.

Naye Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Rais wa Jamhuri ya Namibia. Dkt. Hage Gein amesema kuwa ni lazima nchi wananchama kuhakikisha wanatekeleza Mkakati wa SADC wa kuwa na biashara huru bila vikwazo katika mipaka.

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Watu wa Madagascar, Andry Nirina Rajoelina amesema kuwa anazishukuru nchi za SADC kwa kufanikisha nchi yake kuwa kwenye usalama na utulivu.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 18, 2019
Marais wastaafu watinga katika mkutano wa SADC